Mkuu wa Mamlaka ya Mahakama ya Iran, Hojjatul-Islam Gholam-Hossein Mohseni Ejei, amewatahadharisha watawala wanaoitegemea Marekani na kuamini ahadi za “Shetani Mkuu”, akisema kuwa hawatapata chochote isipokuwa hasara na kushindwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA,-, Mkuu wa Mamlaka ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hojjatul-Islam Gholam-Hossein Mohseni Ejei, amekosoa uungaji mkono wa moja kwa moja unaotolewa na baadhi ya watawala wa eneo kwa Marekani.
Mohseni Ejei amewaonya wale wanaoitegemea Marekani na kudanganywa na ahadi za kile alichokiita “Shetani Mkuu”, akisema kuwa mwisho wao utakuwa ni hasara na kushindwa.
Amesema mtawala anayoiweka ardhi ya nchi yake chini ya matumizi ya Marekani ili kutekeleza uhalifu wa kivita, hatimaye atajuta kwa hatua hiyo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la Mamlaka ya Mahakama nchini Iran, Mohseni Ejei amesema uadui wa Marekani dhidi ya wananchi wa Iran unaendelea, akisisitiza kuwa adui hatabadilisha msimamo wake, bali huibua hila mpya kila anapokaribia kushindwa.
Kwa sababu hiyo, ametoa wito wa kuwa macho daima dhidi ya njama za Marekani, akirejea Operesheni ya Mersad, ambapo adui - utawala wa zamani wa Baath wa Saddam - uliomba kusitishwa kwa mapigano kupitia mpatanishi, huku wakati huohuo ukiandaa na kuzipa silaha kundi la Mujahidiin-e Khalq (MEK)kwa ajili ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran.
Mkuu huyo wa Mamlaka ya Mahakama ya Iran amesisitiza kuwa historia inaonyesha kwamba maadui wanaweza kutumia hila na mbinu mbalimbali wanapokabiliwa na kushindwa, hivyo wananchi na viongozi wa Iran wanapaswa kuendelea kuwa macho na kutokubali kudanganywa na ahadi za maadui.
Maoni yako